Jumatatu , 6th Feb , 2023

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, amesema atazifungia kufanya kazi machijio zote za mkoa wa Dar es Salaam  na nyinginezo hapa nchini  ambazo zimekuwa zikiendesha minada ya mifugo badala ya kufanya kazi husika ambayo ni kuchinja mifugo pekee.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki

Hayo ameyasema Dar es Salaam, wakati akizindua mizani ya mifugo katika mnada wa Pugu ambayo itatumika kupima kilo za mifugo kabla ya kuuzwa.

Waziri Mashimba amesema kufanya hivyo ni kuvunja sheria na ameliomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wafanyabiashara na wafugaji wenyewe kushirikiana ili kubaini machinjio zinazofanya hivyo na kuchukuliwa hatua ikiwemo kufungiwa.

Akizungumza katika uzinduzi huo Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Dkt  Daniel Musa, ameeleza sababu zilizochangia kupanda kwa bei  ya nyama hapa nchini huku Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Amani Mafuru, akieleza mpango uliopo wa kuboresha eneo la Pugu mnadani.