Jumanne , 17th Aug , 2021

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya uchunguzi ili kubaini kwanini uongozi wa Manispaa ya Temeke ulianza kulipa mkopo wa shilingi Billioni 19 miezi miwili baada ya kupokea ilihali mkataba ulionyesha wana-'grace period ya miezi sita.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za Kijichi-Mwanamtoti na Kijichi-Toangoma wilayani Temeke na kituo cha Mabasi kilichopo Buza ambapo amekiri kutoridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo.

"Tunatakiwa tujue hili jengo mkurugenzi gani alikopa bil.19 na kwa ajili ya nini, mkataba ulisema wana grace period ya miezi 6 na kuendelea wao wamelipa mwezi wa pili hela walitoa wapi kabla hawajazitumia zile za mwanzo kwanini waliharakisha kuzilipa na je ziliingia benki, tafuta mweka hazina aliyehusika kwenye kukopa hiyo fedha arudushiwe Temeke kuja kujibu hawezi kuhamishwa huku kuna matatizo" amesema Mhe. Majaliwa.

Pia Mhe. Majaliwa ameshangazwa na na kitendo kilichofanywa na manispaa hiyo ambayo ila wahamisha kwa haraka wale watumishi wenye shida wote huku akitoa agizo la Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kukaa pembeni kwa kile kinachodaiwa kutokuwa na majibu yanayoridhisha.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya ahakikishe anasimamia na anazingatia maslahi ya wana-Temeke katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Wananchi Serikali yenu iko macho kweli kweli na hakuna sarafu itakayotoweka tunailinda na Mawaziri tupo kwa ajili hiyo na tuna maelekezo thabiti ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na watumishi wa umma tupo hapa kuwahudumia wananchi,” amesema Mhe. Majaliwa.