Jumapili , 12th Aug , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Bibi. Pudencis Protas kumkamata Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wa wilaya ya Ruangwa Bw. Anthon Mandai kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Majaliwa ametoa agizo hilo leo Jumapili wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa akiwa katika siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi  wilayani hapo. 

"Huyu Katibu ameshindwa kuwasaidia walimu katika kutatua changamoto zao na badala yake amekuwa akitumia vibaya majina ya viongozi wakuu, ambapo hata mimi alijaribu kutaka kunichakachua kwa kughushi muhtasari wa kikao cha mirathi ya Mwalimu Suwedi Chikawe akitumia jina langu kuwa nilikuwa mwenyekiti wa kikao hicho kilichokuwa na agenda ya kumbadilisha msimamizi wa mirathi aliyeteuliwa na familia jambo ambalo si la kweli", amesema Majaliwa.

Mbali na kukamatwa kwa Bw. Mandai, pia Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Kamanda Pudencis afanye uchunguzi wa kina utakaowezesha kukamatwa kwa mtandao wa watu wote wanashirikiana na kiongozi huyo katika kughushi nyaraka za vikao vya mirathi.

Waziri Mkuu ametoa amri hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa walimu wakimlalamikia kiongozi huyo kuwa na tabia za kudai rushwa, kutowapandisha madaraja, ulevi pamoja na kuwaita walimu hao kwenye vilabu vya pombe kwa ajili ya kuwasikiliza matatizo yao.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma wabadilike na wafanye kazi kwa bidii, waache mazoea na watumie utalaamu wao vizuri katika kuwahudumia wananchi na serikali haitowavumilia wafanyakazi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao.