Jumapili , 18th Nov , 2018

Baada ya kuzungumza na Serikali, makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Afrika, Dkt. Hafez Ghanem amesema kuna masharti wamekubaliana kabla Tanzania haijapewa mkopo wa Dola 300 milioni za Marekani kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.

Makamu wa Rais wa WB Kanda ya Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, akiwa na Rais Dkt. Magufuli, Ikulu jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt.  Ghanem amesema benki hiyo inatoa fedha kwa ajili ya wasichana wote bila kujali hali zao, hivyo kuwatenganisha kwa kigezo cha ujauzito au kingine chochote ni kwenda kinyume na mkakati wa elimu jumuishi.

Wataalamu wetu watashirikiana na serikali kuona ilivyojiandaa kutoa elimu kwa wasichana wote, tutakapojiridhisha bodi ya wakurugenzi itaidhinisha mkopo husika na kuchelewa kwake kutategemea lini serikali itatekeleza masharti tuliyokubaliana", amesema Dkt. Ghanem.

Mkopo huo ilikuwa ujadiliwe na kuidhinishwa Oktoba 30, lakini kutokana na msimamo wa serikali kutotoa fursa ya kuendelea na masomo wasichana wanaopata mimba, bodi ya benki hiyo ilisitisha kuujadili. Kwa utaratibu wa benki hiyo, kabla mradi wowote haujaidhinishiwa fedha zinazohitajika, huujadili kwanza.

Novemba 16, baada ya mazungumzo na makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB), Rais Magufuli alisema kuwa Benki hiyo imeridhia kuipatia Tanzania Dola za Marekani milioni 300 sawa na shilingi bilioni 680.5  kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari, ambapo zitatumika katika ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.