Ijumaa , 24th Mei , 2019

Mwanasheria Mkuu wa Baraza la Mazingira la Taifa NEMC, Vincent Haule amesema wananchi wenye mifuko ya plastiki wanatakiwa kuwasilisha mifuko yao kwenye ofisi za Serikali za mtaa ili kuhakikisha bidhaa hiyo inaondoka mtaani.

Mwanasheria huyo wa NEMC ametoa kauli hiyo akiwa kwenye kipindi cha East Afrilka BreakFast cha East Afrika Radio ambapo amesema msimamo wa Serikali ni uleule kuanzia Juni mosi litakuwa ni kosa kisheria kukutwa na mifuko ya plastiki.

"Kuanzia sasa hivi kama una mifuko ambayo imekatazwa unaweza kupeleka kwenye ofisi za Serikali za Mtaa husika, wao watajua namna ya kuhifadhi na baadaye itachukuliwa kwa ajili ya kuzichoma moto." - amesema Vincent Haule - Mwanasheria NEMC

"Mifuko mbadala iko mingi mfano vikapu, mifuko ya nguo mifuko ya karatasi, watu wasijiulize kuhusu mbadala ya mifuko, na suala la kutunza mazingira sio la muuza duka hata wewe mtumiaji ukienda dukani nenda na kikapu chako" - ameongeza Vincent Haule

Kuanzia Juni mosi 2019, Serikali imepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na kuwataka wananchi watafute mbadala ya mifuko hiyo.