Jumatano , 14th Jan , 2015

Wenyeviti Saba wa mitaa mbalimbali katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, leo wamekula kiapo 'kimya kimya' katika ofisi za halmashauri hiyo zilizopo Magomeni jijini DSM.

Wenyeviti hao ni wale ambao viapo vyao vilizua utata katika zoezi la awamu ya Kwanza lililofanyika Januari 6 baada ya kulalamikiwa na wagombea pamoja na wafuasi wa vyama vya upinzani kuwa hawakushinda wao.

Katika zoezi la Januari 6, kulizuka vurugu kubwa ambapo wenyeviti hao walioapishwa leo walizuiliwa kuingia ukumbini na wengine kupigwa na wafuasi wa vyama vya upinzani.

Walioapishwa leo ni pamoja na :-
Juma Mbena mtaa wa Msisiri A Mwananyamala
Anondumi Mwanga Mtaa wa Mwinjuma Mwananyamala
Hassan Ngonyani Mtaa wa Kawe Mzimuni
Mutani Geta Mtaa wa Ukwamani Kawe
Abinu Issa Mtaa wa Kigogo Kati
Bihamu Abdallah Zangu Mtaa wa Kilunzile
Desdeus Ishengoma Mtaa wa Kibangu.

Mmoja kati ya hawa walioapishwa amedai kuwa alipigiwa simu saa 6 usiku na kutakiwa kufika ukumbini hapo kwa ajili ya kuapishwa.

Wadau wengine katika maeneo hayo wakiwemo viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani wanadai kuwa hawakuwa na taarifa ingawa walisikia kuwa wenyeviti hao wangeapishwa katika mitaa yao na si katika ofisi za halmashauri.

Zoezi la kuwaapisha limechukua muda usiozidi dakika 20, huku likihudhuriwa na wapambe wasiozidi 50.