Alhamisi , 22nd Jul , 2021

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema itajulisha umma sababu ya vifo vya samaki waliokutwa wakielea kwenye ufukwe wa bahari Jijini Dar es Salaam mara baada ya kupatikana kwa majibu ya uchunguzi wa kimaabara unaofanywa hivi sasa.

Picha ya samaki (picha kutoka mtandaoni)

Taarifa ya Wizara hiyo imesema tarehe 21 mwezi Julai, 2021 saa 3:30 asubuhi, ofisi ndogo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mkoa wa Dar es Salaam ilipokea taarifa kutoka kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala kuhusu tukio la kuelea kwa samaki waliokufa katika ufukwe uliyopo karibu na Hospitali za Agha Khan na Ocean Road Jijini Dar es Salaam.

Samaki waliokusanywa ni kiasi cha Kilogramu 164 na kufikisha Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambazo sampuli zao zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kubaini sababu za vifo vya samaki hao, huku kiasi cha Kilogramu 156 kilichosalia kilikabidhiwa kwa afisa uvuvi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuteketezwa ambalo lilishuhudiwa na maafisa na wizara.

Kufuatia tukio hilo Wizara imewaasa wananchi kuendelea na biashara ya samaki katika masoko ya Jiji la Dar es Salaam kama ilivyo kawaida na kutoa shukrani kwa wananchi wote kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha uliofanikisha kuzuia kuingizwa kwa samaki hao sokoni na hatimaye kuteketezwa.