Jumatano , 10th Feb , 2021

Wizara ya Elimu imekanusha waraka wa tahadhari juu ya virusi vya Corona uliotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Prof. Elifas Bisanda, na kwamba tahadhari hiyo ni maoni yake binafsi na haikuzingatia mwongozo wa tahadhari kama hiyo uliotolewa na Wizara ya afya Mei, 2020.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa Wizara ya Elimu Oliva Kato, na kueleza kuwa waraka huo batili wa Profesa Bisanda ulitolewa Februari 8, 2021, na kwamba Wizara inawaelekeza wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho kuendelea na masomo na kazi zao kama kawaida.

Mbali na agizo hilo Wizara ya Elimu pia inatoa rai kwa taasisi zote za elimu nchini kuzingatia maelekezo ya serikali kuhusu udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona na kutoa onyo kwa viongozi na watumishi wa Wizara ya Elimu kuacha kutumia nembo za serikali wanapotoa maoni yao binafsi.