Jumanne , 2nd Sep , 2025

Rais Xi Jinping, pamoja na wenzake wa Urusi Vladimir Putin na Mongolia Ukhnaa Khurelsukh, wamefanya mkutano wa saba wa wakuu wa nchi hizo tatu leo asubuhi ya tarehe 2 Septemba, kwenye Jumba la Mikutano ya Umma mjini Beijing.

Katika mkutano huo Xi Jinping amesifu kuimarika kwa ushirikiano wa pande tatu kati ya China, Urusi na Mongolia katika miaka ya hivi karibuni na ametoa mapendekezo matatu ya kukuza ushirikiano kati ya mataifa hayo yaani kuimarisha hali ya kuaminiana kisiasa, kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana, na kuimarisha ushirikiano ndani ya utaratibu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO.

Kwa upande wake, rais Putin amesema kuwa Urusi, China na Mongolia ni majirani wema na wenye desturi ya muda mrefu ya ushirikiano. Kuimarisha kuaminiana kisiasa ni muhimu na kutasaidia kuimarisha msingi wa uhusiano wa pande tatu.

Naye rais Khurelsukh amesema Mongolia imejizatiti katika kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili, kupanua ushirikiano wa pande tatu, kuendeleza ujenzi wa Ushoroba wa Kiuchumi wa China-Mongolia-Urusi, na kuimarisha mawasiliano ya kitamaduni ili kuwanufaisha watu wa nchi hizo tatu na kuhimiza maendeleo na ustawi wa kikanda.

Ameongeza kuwa mwaka huu ni kumbukizi ya miaka 80 ya ushindi wa Vita vya Watu wa China dhidi ya Uvamizi wa Japan na Vita Vikuu vya Kizalendo vya Umoja wa Kisovieti. Watu wa Mongolia, China na Urusi wanapaswa kusherehekea na kuadhimisha kwa pamoja wakati huu wa kihistoria na kukuza mtazamo sahihi wa historia ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.