Z Anto amlalamikia Paul Makonda

Jumanne , 13th Feb , 2018

Msanii wa muziki wa Bongo fleva, Z Anto ameweka wazi kuwa wapo watu wanatumika sasa kwa lengo la kutaka kumchafua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda na kujinufaisha katika migogoro ya ardhi kupitia kampeni ya Mkuu wa mkoa.

Z Anto amesema hayo wakati akifanya mahojiano na kituo kimoja cha habari na kudai kuwa yupo mtu ambaye anajiita Sajenti Mohammed Alli ambaye alifika nyumbani kwao na kuwaeleza kuwa ametumwa moja kwa moja na Paul Makonda na kusema kuwa Mkuu huyo wa mkoa analihitaji eneo hilo la kina Z Anto. 

"Ombi langu kwa Mhe. Makonda kuhusu hii oparesheni iliyopo sasa namweleza tu kuna watu wanatumia mgongo wake kuchafua hali ya hewa na kumchafulia jina pia hata yeye mwenyewe maana kama mtu anakuja anasema kuwa yeye ametumwa moja kwa moja kutoka kwa Makonda na kwamba Makonda amempa agizo kuwa analihitaji eneo letu. kitu ambacho tumeulizia wilayani hakifahamiki, serikali za mitaa hakijulikani, polisi hakijulikani hata kwa baadhi ya watu ambao wapo karibu na Mkuu wa mkoa pia hawafahamu hiki kitu, hivyo ina ashiria kwamba kuna michezo michafu na watu wanataka kutumia oparesheni hii ya Mhe. Makonda kufanya yale wanataka kufanya" 

Aidha Z Anto alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwasihi Wanasheria mbalimbali ambao amewatuma katika oparesheni hiyo ya kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi kuwa wasisikilze maneno tu bila kupata uhakika wa nyaraka mbalimbali. 

Familia ya Z Anto imetuhumiwa kudhulumu kiwanja kitu ambacho Z Anto amekipinga na kusema kuwa watu ambao wameibuka na kusema wamedhulumiwa kiwanja hicho wao hawawatambui na kudai kuwa kiwanja chao hicho kilikuwa na kesi kwa miaka 19 iliyopita lakini wao walishinda kesi hiyo na hao walioibuka sasa kudai ndiyo wamiliki wa eneo hilo wao hawawatambui.