Jumanne , 22nd Mei , 2018

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kukubali amekosea na kurejea katika utaratibu wa awali wa utoaji wa vibali vya vitalu vya uwindaji. 

Akichangia bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2018/19 ambayo ni Sh115.8bilioni, Zitto amesema:, “Waziri kwa kuwa umeona kuna tatizo la kisheria na maagizo uliyoyatoa ni kinyume na sheria turejee katika utaratibu wa awali.” 

Zitto katika hatua nyingine ametoa wito kwa wizara husika kutafakari upya suala la kuondoa miti katika hifadhi ya Sealou kwani kwa kufanya hivyo kutaathiri mazingira kwa kiasi kikubwa.

“Hakuna anayekataa maendeleo ya taifa letu lakini kwa kuondoa miti ile kutaathiri mazingira pamoja na kupoteza watalii, tunaomba zoezi hili lisimame kwanza tutafakari athari zake ndio uamuzi ufanyike”. Amesema Zitto.