Jumanne , 13th Jul , 2021

Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula ameagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa maafisa wa ardhi watatu ambao walihamishiwa kikazi Wilayani Kilosa miaka miwili iliyopita ambapo tangu wahamishiwe wilayani humo hawajawahi kuonekana kazini.

Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula

Naibu Waziri huyo ametoa agizo hilo akiwa mkoani Morogoro kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi,  ambapo ametoa maelekezo kwa kamshina wa ardhi kuanza kuchukua hatua kwa maafisa hao na kwamba serikali haiwezi kuendelea kuwa na watumishi ambao hawapo kwenye vituo vyao vya kazi huku wananchi wakishindwa kutatuliwa changamoto zao

“Nimemuelekeza kamishna ili aweze kuanza taratibu zinazotakiwa kupitia ofisi ya katibu mkuu ambaye ndiye mwenye dhamana na ajira yao na mamalaka ya nidhamu ili hatua za nidhamu kwa watu hawa ziweze kuchukuliwa hatuwezi kuendelea kuwa na watu ambao tunawahesabuwako Wilaya ya Kilosa alafu Kilosa hawapo, alafu huku migogoro ni mingi isiyoisha kumbe kuna watumishi ambao hawajafika kwahiyo hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa hawa watu watatu” amesema Mhe. MMabula

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema watahakikisha wanakomesha migogoro inayosababishwa na baadhi ya watu wasiowaadilifu pamoja na kuunda tume ya wataalam ya kubainisha mipaka ya vijiji huku Kamishna wa Ardhi Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro Frank Mizikunte akasema wataanzisha zoezi la urasimishaji ardhi ilikuepukana na migogoro ya ardhi inayojitokeza.