Alhamisi , 16th Aug , 2018

Star wa muziki nchini Uganda, Jose Chameleone amemuandikia barua ya wazi Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni kwa lengo la kumuombea msamaha msanii mwenzake, Robert Kyagulanyi 'Bobi Wine' ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi hadi hivi sasa kwa tuhuma za uchochezi.

Jose Chameleone akiwa katika picha ya pamoja na Bobi Wine.

Chameleone ameandika barua hiyo kupitia ukurasa wake wa kijamii leo Agosti 16, 2018 ikiwa imepita siku chache tangu dereva wa Bobi Wine ambaye pia Mbunge wa Kyadondo Mashariki, kuuawa kwa kupigwa risasi katika vurugu wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Arua .

"Mh. Kyagulanyi amekuwa akishirikiana na mimi pamoja na jamii yote kuwaweka wananchi wa Uganda huru dhidi ya sauti za kigeni, tumeuza muziki wetu nje ya mipaka kupitia pesa zetu. Bobi Wine amezuiliwa shughuli zake za kiutawala, 'just like any young ambitious man, he has treaded a path of aggressiveness", ameandika Chameleone.. 

Pamoja na hayo, Chameleone ameendelea kwa kusema kuwa "ukiwa kama baba kiongozi wa taifa, ukubwa huo utuongoze sisi kwa mfano wa kusamehe na majadiliano ikiwa hilo ndilo tatizo kubwa linaloikumba jamii yetu, tunaomba msamaha. Ni mtoto wa taifa hili kama kauli mbiu inavyosema 'Kwa Mungu na nchi yangu' kwa heshima zote tunaomba Rais wetu umsamehe katika kipindi hiki, wote tunakosea lakini mtu mzuri ni yule anayesamehe.Mh. Rais Museveni, wewe ni baba, mzazi na mtu wa kusamehe. Wote tunatulia sasa tuna imani kuwa huko mbeleni tutaishi katika nchi ya amani na upendo".

Kwa upande mwingine, mashabiki na wananchi wa Uganda wamemtaka Jose Chameleone asiishe kutoa hisia zake kwenye mitandao ya kijamii pekee bali atafute njia ya kukutana na Rais Museveni, kusudi wazungumza uso kwa uso kuhusu tatizo hilo licha ya uwezekano mdogo wa kukutana na kiongozi huyo.