Jumanne , 21st Jul , 2015

Vituo namba moja kwa vijana vya East Afrika Television (EATV) pamoja na East Africa Radio kwa kushirikiana na wasanii wa kundi la Weusi leo vimezindua rasmi wimbo wa Zamu Yako.

Nikki Wa Pili akiongea katika mkutano na waandishi wa habari

Wimbo huo ulioimbwa na wasanii hao ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya Zamu Yako 2015 ya kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwa upande wao wakiongelea kuhusu wimbo huo uliotengenezwa na producer Nahreel, mmoja wa wasanii wa kundi la Weusi, Niki wa Pili, amesema vijana wanawajibu wa kushiriki kikamilifu katika kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki zoezi la kupiga kura ifikapo Oktoba 25 mwaka huu.

Katika uzinduzi huo Kaimu Mkuu wa Masoko Alex Galinoma amesema uzinduzi wa wimbo huo ulioimbwa na kundi la Weusi linalokubalika mno kwa sasa nchini, unaonesha ni kwa jinsi gani wasanii wa kundi hilo walivyokuwa na moyo wa kurudisha kwa jamii kwa kutumia vipaji vyao kutoa elimu ya bure kwa umma.

Kampeni ya Zamu Yako 2015 ilizinduliwa na kituo cha East Afrika Television (EATV) pamoja na East Africa Radio, Februari 11 mwaka huu, katika kuhakikisha vijana wanashiriki kikamilifu kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, kushiriki kuwania nafasi za kisiasa na kuwachagua viongozi makini wakati wa kupiga kura.