Jumanne , 10th Dec , 2019

Bondia Andy Ruiz Jr 'kibonge mwepesi' mwenye uraia wa Mexico na Marekani, amesema kuwa kuongezeka uzito pamoja na kula bata zaidi na marafiki zake, ndiyo sababu kubwa iliyopelekea yeye kuchezea kichapo mbele ya Bondia Anthony Joshua.

Bondia Andy Ruiz na Anthony Joshua wakiwa ulingoni.

Andy Ruiz amesema hayo alipodakwa na kamera za mtandao wa TMZ, wakati anashuka katika Airport ya jiji la Los Angeles Marekani, siku ya Desemba 9, 2019.

"Nahisi nilikuwa nakula kila kitu ndiyo maana nimeongezeka uzito, nilikula sana bata na kufurahia maisha na marafiki zangu pamoja na kunywa vinywaji vya Corona, kwa hili umbo itabidi nifanye mazoezi nchini Mexico na jijini California na nitalichukulia hili jambo kwa umakini zaidi" amesema Andy Ruiz.

Aidha amesema kwa sasa ana mpango wa kuweka kando mambo ya kula bata na marafiki zake, pia ametenga muda wa kukaa na familia yake huku akifanya mazoezi kwa ajili ya pambano la tatu na anataka kurudisha mikanda yake iliyoenda kwa Anthony Joshua.

Katika pambano lake la raundi ya pili alilopigana siku ya Desemba 7, 2019, Andy Ruiz alikuwa na kilo 284,na kwamba ameongezeka kilo 15 tofauti na zile za mwanzo, alipopigana na Anthony Joshua katika pambano lake la kwanza mwezi Juni, lililompatia ushindi wa KO katika raundi ya 7.