Mama Nandy aikataa ndoa ya Billnass na Mwanaye

Jumanne , 4th Aug , 2020

Mama wa msanii Nandy,  Maria Charles Mfinanga, amesema kwa sasa Billnass na Nandy bado ni watafutaji hivyo watulie na wajipange hadi wafikie malengo, kisha ndiyo waingie kwenye suala la ndoa.

Mama Nandy upande wa kushoto, Billnass na Nandy upande wa kulia

Akipiga stori na EATV & EA Radio Digital, Mama Nandy amesema wakiingia kwenye ndoa kuna watoto na kuanzisha familia, hivyo itawarudisha nyuma kibiashara.

"Bado wote ni watafutaji, wasogee kwanza kutimiza malengo kisha waingie kwenye ndoa, ndoa ipo tofauti siyo kama unafanya vitu vyako mwenyewe, wapo pamoja na wanashirikiana kwa vitu vingi hivyo wakae wajipange, ukiingia kwenye ndoa kuna kupata watoto na kuanzisha familia hivyo kibiashara wanaweza kurudi nyuma" amesema Mama Nandy.

Pia Mama Nandy amesema, anajua walifanyiana surprise ya kuvalishana pete ila wao kama wazazi pete lazima itarudiwa na wakitaka kuoana michakato mingine itaanza upya.