Jumamosi , 31st Mei , 2014

Aliyekuwa Mtayarishaji Vipindi na Muongoza filamu maarufu, Marehemu George Tyson anatarajiwa kusafirishwa wiki ijayo kwenda nchini Kenya kwaajili ya maziko.

Marehemu George Tyson

Taarifa hizi ni kwa mujibu wa ndugu wa Marehemu, Bwana Benson Hukumu ambaye pia ameeleza juu ya kuwasili kwa mwili wa Marehemu kutoka Morogoro jioni ya leo.

George Tyson amepoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Gairo akiwa safarini kurejea Dar es Salaam akiwa na timu ya kipindi cha The Mboni Show.

Sababu ya ajali hii imeelezwa kuwa ni tairi ya gari kupasuka na kusababisha gari kupoteza muelekeo na kupinduka, ikiwa na watu nane ndani yake ambapo George peke yake ndiye aliyepoteza maisha na wengine kujeruhiwa.

Kwa wale wote waliokuwa na wasiwasi juu ya hali ya Mtangazaji wa kipindi Mboni Masimba, wanatakiwa kufahamu kuwa mtangazaji huyu hakuwa katika gari iliyopata ajali na yupo salama akiendelea kukabiliana na mshtuko na huzuni kubwa kutokana na tukio hili.