Jumatano , 23rd Jan , 2019

Staa wa muziki wa Jazz, Oliver Mtukudzi amefariki dunia mchana leo Januari 23, 2019 huko mjini Harare Zimbabwe. Mtukudzi amefariki akiwa na miaka 66.

Oliver Mtukudzi enzi za uhai wake

Taarifa za kifo cha Mtukuzi zimethibitishwa na record label yake ya Gallo Record Company huku wakishindwa kuweka wazi juu ya ugonjwa ambao umepelekea kifo cha nguli huyo wa muziki.

Wabunge mbalimbali wa Zimbabwe wametoa pole kwa familia na mashabiki wa Mtukudzi huku pia wakimtaka Rais kutangaza msiba wa kitaifa.

"Tumepoteza nembo ya taifa, namwandikia Rais Emmerson Mnangagwa kuomba atangaze msiba wa taifa kwa heshima ya shujaa huyu kwa mchango wake wa kitaifa kwenye sekta ya muziki, sanaa na utamaduni'', amesema Mbunge wa Norton Temba Mliswa.

Moja ya viongozi wengine waliotoa pole ni Waziri wa zamani wa Elimu, Michezo, Sanaa na Utamaduni nchini Zimbabwe David Coltart ambaye amesema "Pumzika kwa amani Oliver Mtukudzi, kama kuna mtu yeyote amewahi kuitangaza Zimbabwe ni wewe. Asante kwa kutufanya tufurahi kwa muda mrefu."

Mtukudzi maarufu kama Tuku alikuwa ni msanii na mwandishi mashuhuri wa ngoma mbalimbali huku akiwa ni moja ya wasanii wenye albam nyingi zaidi akiwa nazo zaidi ya 60.

Mapema mwaka jana alilazwa katika hospitali moja mjini Harare kwa shinikizo la moyo. Hata hivyo aliruhusiwa na hali yake ikaimarika.