Nuh Mziwanda adai kupelekwa kwa mganga na Shilole

Jumatatu , 9th Dec , 2019

Msanii na mtayarishaji wa muziki, Nuh Mziwanda, amefunguka madai ya kuchukuliwa nyota ya kimuziki na kimaisha, pamoja na suala la kupelekwa kwa mganga na aliyewahi kuwa mpenzi wake Shilole.

Msanii Shilole akiwa na Nuh Mziwanda.

Kupitia EATV & EA Radio Digital, Nuh Mziwanda, amewajibu mashabiki ambao wanadai amechukuliwa nyota yake na mpenzi wake huyo wa zamani kwa kusema, hajui kama amechukuliwa nyota yake ila anachojua alikuwa kimya kwa muda mrefu.

"Kama mashabiki wanahukumu hivyo ni sawa ila ukimya wangu nilikuwa bize narekodi, kufanya kazi, mimi naona nipo sawa nafanya mambo yangu kimpango wangu pia siamini katika vitu kama hivyo ila kama watu wanaamini sawa labda wao wanamjua yule bi Dada kama ni mchawi mchawi" amesema Nuh Mziwanda.

Aidha kupitia kipindi cha DADAZ ya East Africa Television, Nuh Mziwanda, ameeleza kuwa aliwahi kupelekwa kwa mganga na Shilole.

"Wakati naachia wimbo wa jike shupa aliniambia niende kwa mganga, ili nijue nyimbo gani kali naiachia baada ya jike shupa pia akamtumia rafiki yangu Beka ili anishawishi kwenda kwa mganga na nilivyokubali tu kesho yake asubuhi alinifata tukaingia kwenye gari akanipeleka kwa mganga Tanga" ameeleza.