Single Mtambalike adai siyo kila mzuri aigize

Alhamisi , 28th Nov , 2019

Muigizaji wa filamu nchini, Single Mtambalike, ameibuka na kusema kuwa sio kila mwanamke au mwanaume mwenye muonekano mzuri, lazima aingie katika fani ya uigizaji wa filamu kwa sababu ya kutumia uzuri wake.

Picha ya msanii wa filamu Bongo,Single Mtambalike.

Mtambalike amefunguka hayo kupitia EATV & EA Radio Digital, ambapo amesema uigizaji unahitaji uwezo mkubwa na ujuzi na si muonekano wa mtu.

"Hilo ndilo lililopelekea hadi kufikia hapa sasa kwa sababu watu waliamini kwamba, watu wenye mionekano mizuri wakikaa mbele ya kioo basi filamu itauza au wakikaa mbele ya filamu na kuwa maarufu itafanya vizuri ila kwangu mimi sipo huko huwa naamini katika 'perfomance' na muigizaji yeyote ni kinyago" amesema Single Mtambalike.

Aidha Mtambalike ameongeza kuwa "Kama kinyago chako kikikaa vizuri basi utakuwa unaweza kuuvaa uhusika wowote ule na sio lazima uwe mzuri pia kama utakuwa na uwezo wa kufikiri kwa kumsikiliza na kumuelewa muongozaji alichomaanisha, unaweza ukawa muigizaji mzuri sana" ameongeza.

Pia amesema kuwa ili mtu aigize, lazima afuate misingi na miiko ya fani hiyo na ajue vitu anavyotakiwa kuvifanya na asivyotakiwa kuvifanya.