Wasanii Afrika Mashariki waomboleza msiba wa Mengi

Alhamisi , 2nd Mei , 2019

Kundi la wasanii wa muziki kutoka nchini Kenya Sauti Sol, limeungana na Afrika nzima kuombeleza msiba wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dr. Reginald Mengi.

Kushoto ni kundi la Sauti Sol na Mwana FA kulia.

Sauti Sol wameeleza namna ambavyo Afrika imepoteza mtu muhimu aliyesimama kama mtu mwenye maono, mjasiriamali, mwandishi wa vitabu pamoja na baba wa watu wengi kwa namna alivyojitoa kusaidia watu.

''Twajivunia kuwa ulikuwa baba mlezi wa wengi. Pumzika baba. Ndugu zetu wa Tanzania tuko pamoja'' wameandika Sauti Sol.

Pia wameungana na wasanii wenzao wa Tanzania ambao nao wameguswa na msiba huo na kwa pamoja wametoa salamu za rambirambi kwa kueleza msaada wa Dr. Mengi katika kiwanda cha muziki na burudani kwa ujumla.

Wasanii Alikiba, Shetta, Lady Jay Dee, Nandy, Ruby, Fid Q, Billnass, Barnaba pamoja na wengine wengi wameguswa na msiba huku wakitumia mitandao ya kijamii kutuma salamu za rambirambi.

Kwa upande wake msanii Mwana FA ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), ameeleza haya, ''Ukapumzike kwa amani mzee wetu. Umetekeleza kilichokuleta Duniani,na tumeona. Umeacha alama''.