Alhamisi , 21st Mar , 2019

Mtoto mkubwa wa Marehemu Ephraim Kibonde anayejulikana kwa jina la Ephraim Jr, ameweka wazi jinsi ndoto yake kubwa itakavyoanza kukosa muelekeo, kutokana na kifo cha baba yake.

Akizungumza siku chache baada ya msiba, Ephraim amesema kwamba alikuwa na ndoto ya kuja kuwa mcheza soka mkubwa kama alivyo Mbwana Samatta, na alishawahi kumwambia baba yake amsaidie katika kutimiza ndoto hiyo, na ahadi aliyompa ilikuwa aitekeleze mara baada ya kurudi msibani Bukoba.

Ephraim ameendelea kuelezea kwamba alipomueleza baba yake juu ya ndoto yake ya kuwa mcheza soka, baba yake alimtaka aendelee kufanya mazoezi, na wakati ukifika basi atamsaidia kumuungansiha na timu yoyote ili aanze safari yake ya kuwa 'Mbwana Samatta'.

Asimulia alivyoahidiwa na baba yake

 

“Mimi napenda sana mpira, na nilikuwa na ndoto kubwa za kufika mbali, kama alivyo Mbwana Samatta vile, baba aliniambia niendelee na mazoezi kwa sasa, kwani hivi vitu vinaweza vikashughulikiwa wakati timu ziko mapumzikoni, nilikuwa naendelea na mazoezi na nikiweka imani kubwa, na aliniambia nimkumbushe mara kwa mara, hata alivyosafiri aliniahidi akirudi Bukoba atalishughulikia”, amesema Ephraim.

Ephraim ameendelea kwa kusema kwamba licha ya kwamba anajuana na marafiki wengi wa baba yake wanaofahamu masuala ya soka, lakini kwa sasa hajalipa tena kipumbele, kwani anahisi wadogo zake wanamuhitaji zaidi.

“Kwa sasa sijapata muda wa kukaa nao na kuwaambia, kwani sijalitilia maanani sana kwa sababu naona wadogo zangu wananihitaji zaidi”, amesema Ephraim Jr

Ephraim Kibonde ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watatu walioachwa na Mtangazaji maarufu Ephraim Samson Kibonde, aliyefarikia Machi 7, 2019, baada ya kuugua ghafla.