Jumatano , 1st Mei , 2019

Mtoto wa miaka mitano mkazi wa Dodoma ambaye alipatwa na tatizo la kutokwa na damu sehemu za siri (hedhi) anatarajiwa kutolewa kizazi ili kuokoa uhai wake.

Kwa mujibu wa mama mzazi wa mtoto huyo, Bi. Loveness Samwa amesema kwamba mtoto wake huyo ambaye kwa sasa yuko hospitali ya Taifa ya Muhimbili akipatiwa matibabu, anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa kuondoa kizazi chake, ili kuzuia madhara zaidi yaliyotakana na kuvuja kwa damu.

Bi. Lovenes amesema kwamba baada ya kufika Muhimbili wakitokea Dodoma, binti yake akiwa amezidiwa, alipokelewa na kuanza kuhudumiwa, na mara baada ya vipimo ndipo akapewa majibu ambayo yatalazimu mtoto wake kutolewa kizazi.

"Tulifika hapa Muhimbili saa 4 asubuhi, madaktari walivyotuona wakaanza kumtibia kwanza mwanangu kwa sababu alikuwa bado hajapata fahamu, walimchukua na kuanza kumfanyia vipimo ambapo wakati nasubiria majibu walimtundikia maji wakamuwekea na Oxygen ambapo alikuja kuzinduka saa 11 jioni. Daktari aliniita tena kwa ajili ya kunipa majibu ambapo aliniambia kwamba kipindi mtoto wangu anapata siku zake, kuna damu ilienda kuganda kwenye kizazi, hivyo kusababisha kiharibike, kwa hiyo anatakiwa afanyiwe upasuaji ili kuondoa kizazi kwa lengo la kuokoa maisha yake", amesema Bi. Loveness.

Hata hivyo mama huyo amesema kwamba ili mtoto wake aweze kufanyiwa upasuaji anatakiwa alipie pesa shilingi laki nne, pesa ambayo amedai kuwa hana, na hata alizoanzia matibabu alichangiwa na watu.