Alhamisi , 17th Jan , 2019

Tarehe 16, Januari ya kila mwaka ni sikukuu ya kidini ya kutakasa wanyama kwa kuwapitisha juu ya moto mkali, inayofanyika na mamia ya wakazi wa miji mbalimbali nchini Hispania.

Waendesha farasi wakivuka katika moto mkali

Sherehe hiyo inayojulikana kama siku ya ' Saint Anthony' au sherehe ya 'Luminarias', hufanyika kwa kuwasha moto wenye moshi na kisha mamia ya wakazi hao hupita katika moto wakiwa juu ya wanyama hao kwaajili ya kuwatakasa.

Wanyama ambao mara nyingi hupitishawa katika moto ni farasi, ambapo licha ya kuwatakasa, pia hupitishwa juu ya moto huo kwaajili ya kuwalinda na matukio mbalimbali mabaya, wakiamini kuwa ni wanyama ambao hawapaswi kutendewa vibaya.

Sherehe hiyo ni muendelezo wa muda mrefu wa tamaduni za nchi ya Hispania, ambapo inakadiriwa kuwa ilianza kufanyika tangu miaka 500 iliyopita, ambapo hufanyika katika mji mdogo wa San Bartolome de Pinares unaopatikana Kilomita 100 kutoka Mji Mkuu wa nchi hiyo, Madrid.

Sherehe ya mwaka huu iliyofanyika jana, Januari 16, jumla ya farasi 120 pamoja na waendeshaji wao walipita katika moto huo mkali huku maelfu ya watu wakifurahia kwa kunywa pamoja na kucheza  hadi usiku, ikiwa ni katika kuadhimisha siku hiyo.