Sherehe za 'Birthday' kuanza kulipiwa mwezi ujao

Ijumaa , 25th Jan , 2019

Imeelezwa kuwa viwango vya tozo kwa vibali vya shughuli au sherehe zote za kijamii kwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, vitaanza kutozwa shilingi elfu hamsini kuanzia Februari mosi.

Kupitia barua iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Rugambwa Banyikila, imeeleza kuwa hivyo ndio vitakuwa viwango vipya ambapo vitahusisha hadi sherehe za kumbukizi za siku ya kuzaliwa 'birthday party'.

"Kuanzia tarehe mosi Februari 2019, shughuli za kupiga muziki, harusi, Jando na unyago, birthday, Send-Off na shughuli nyingine zinazoendana na hizo zitalipiwa sh. 50,000 kwaajili ya kupatiwa kibali", imesema taarifa iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi huyo.

Ulipotafutwa uongozi wa Manispaa hiyo ili kutoa ufafanuzi, kuhusu barua hiyo na muongozo huo uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ulidai upatiwe muda utatoa ufafanuzi.