Wasiokula mbogamboga hatarini kuugua magonjwa haya

Jumapili , 20th Jan , 2019

Ni kawaida sana kusikia mtu akiagiza chakula hotelini au mgahawani, akisema kuwa asiwekewe mbogamboga kwasababu tuu hakuzoea kula, wengine wakidai kuwa hawaoni ladha na wengine wakidai kuwa hawajakua katika maisha ya kula mbogamboga.

Mbogamboga na matunda

Inaelezwa kuwa raia wengi wa bara la Afrika hawazingatii ulaji wa virutubisho mbalimbali vya mwili, sababu zikiwa ni umasikini, kukosa elimu ya lishe bora pamoja na uhaba wa mbogamboga katika maeneo mengi hasa yaliyo na ukame.

Mbogamboga na matunda zimesheheni vitamini na virutubisho muhimu sana katika afya ya binadamu. Kwa mujibu wa mtafiti, Laura Moore wa Chuo Kikuu cha Afya cha Texas, hata kama unaweza kupata virutubisho vingi kutoka vyakula vingine, lakini bado mwanadamu anaweza kupata magonjwa mbalimbali kutokana na kukosa virutubisho vitokanavyo na mbogamboga na matunda.

Zifuatazo ni dalili ambazo zinaweza kukuonesha kuwa una upungufu wa vitamini zitokanazo na matumizi hafifu ya vyakula vya mbogamboga na matunda.

Matatizo ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula

Kutopata mbogamboga na matunda ya kutosha kunaweza kusababisha matatizo ya mmeng'enyo wa chakula tumboni kama vile kuganda kwa chakula tumboni (Constipation) na kupelekea ugumu wa mmeng'enyo. Hii ni kwasababu mboga mboga na matunda vina kambakamba ambazo husaidia kuongeza uzito wa kinyesi na kupitisha kwa urahisi.

Hupunguza hatari ya ugonjwa wa Kansa

Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Kansa ya Marekani (AICR), chakula pekee kinachoweza kupunguza hatari dhidi ya kansa kwa mwanadamu ni lishe iliyosheheni vyakula vya mbogamboga na matunda. vyakula hivyo vinazalisha virutubisho visivyo na sumu kama Vitamin E na Vitamin C ambavyo hupunguza hatari ya kansa.

Kuongezeka kwa hatari ya shinikizo la damu

Mwanadamu akila vyakula vingi vya madini ya sodium bila kuzingatia matumizi ya mbogamboga na matunda hupelekea shinikizo la damu. Utafiti pia unaonesha kuwa mwanadamu mwenye shinikizo la damu anaweza kupunguza kiwango hicho kwa kutumia mbogamboga na matunda zaidi kuliko matumizi ya madawa.

Hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo

Pale ambapo shinikizo la damu huwa chini, kula vyakula vya mbogamboga na matunda inaweza kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na kiharusi yanayoweza kusababishwa na tatizo hilo. Mboga mboga na matunda havina 'Cholesterol' kwahiyo kutumia sana vyakula hivi humsaidia mtu kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na kiharusi.

Kuongezeka kwa uzito

Kutojali vyakula vya mbogamboga na majani pia kunasababisha mwanadamu kuongezeka uzito kwasababu atakuwa anatumia vyakula vyenye mafuta na kalori. Vyakula vya mbogamboga na matunda havina mafuta na kalori kwahiyo endapo mtu atazingatia zaidi katika mlo wake, atakuwa salama zaidi katika kuzuia kuongezeka kwa uzito.