Jumatano , 31st Mar , 2021

Shirikisho la soka Africa ya kusini 'SAFA' limemfuta kazi aliyekuwa kocha wake wa timu ya taifa Bafana Bafana Molefi Ntseki baada ya kushindwa kufuzu michuano ijayo ya AFCON inayotazamiwa kufanyika mwaka 2022 nchini Cameroon.

Aliyekuwa kocha wa Bafana Bafana Molefi Ntseki

Hatua hiyo toka SAFA imetangazwa leo katika  makao makuu yake mjini Johannesburg kufuatia kipigo cha bao 2-0 kutoka kwa Sudan  katika mchezo wa mwisho wa makundi uliyotoa hatma yao.

Uteuzi wa Molefi Ntseki mwaka 2019 ulipokelewa kwa wasiwasi na wadau wengi hasa uzoefu mdogo aliyokuwa nao japo alikuwa msaidizi wa muda mwingi wa aliyekuwa kocha wao Stuart Baxter ambaye aliiongoza Bafana Bafana hadi hatua ya robo fainali kwenye AFCON iliyopita 2019 nchini Misri.

Bafana Bafana mabingwa wa mwaka 1996 wamekuwa washindani wazuri katika michuano mbalimbali ukanda wa Africa na Dunia nzima kiujumla tangu warejee kushiriki michuano tofauti tofauti ya soka mara baada kuondolewa vizuizi kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi nyakati hizo.

Africa kusini ilikuwa kundi C imemaliza ikiwa na alama 10 nyuma ya Sudani mwenye alama 12 na kinara wa kundi Ghana yenye alama 13 huku Sao Tome and Principle wakiburuza mkia bila alama yeyote kibindoni.