Jumapili , 18th Nov , 2018

Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewatakia mchezo mwema timu ya taifa 'Taifa Stars' katika mchezo wake wa kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika 'AFCON' dhidi ya Lesotho.

Rais Magufuli

Rais Magufuli amewatakia mchezo mwema pamoja na kuwapa maagizo ya kurejea nyumbani na ushindi katika mchezo huo, ushindi ambao utaandikisha historia katika nchi.

"Vijana wangu Taifa Stars, muda mfupi ujao nitakuwa nikitazama mchezo kati yenu na timu ya taifa ya Lesotho, mimi na Watanzania wenzangu tunawatakia mchezo mwema, mrudi na ushindi," ameandika Rais Magufuli katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Ikumbukwe mwezi uliopita, Rais Magufuli alichangia sh. milioni 50 kwa Taifa Stars kwaajili ya maandalizi yake katika michezo yake miwili ya mwisho ya kufuzu katika michuano hiyo huku akisisitiza kuwa huu ndio wakati wa timu hiyo kufuzu katika michuano mikubwa ya Afrika na Dunia kwa ujumla.

Endapo Taifa Stars itafanikiwa kupata ushindi katika mchezo wa leo, itajikatia tiketi ya moja kwa moja ya kufuzu michuano hiyo ambayo itafanyika nchini Cameroon mwaka 2019.