Ijumaa , 11th Oct , 2019

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Oktoba 7, 2019 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya uamuzi ufuatao,

Ibrahim Ajibu kwenye moja ya mechi za Simba

VIWANJA

Kamati imezuia baadhi ya viwanja kutumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutokana na kuwa na upungufu katika maeneo mbalimbali ikiwemo la kuchezea (pitch) na uzio wa ndani unaotenganisha wachezaji na washabiki (fence).

Viwanja hivyo ni Kinesi Bull (Dar es Salaam), Bandari (Dar es Salaam), Jamhuri (Morogoro), Namfua (Singida), na Mkwakwani (Tanga). 

Klabu ambazo timu zao zinatumia viwanja hivyo zimepewa nafasi ya kufanya marekebisho kipindi hiki ambacho Ligi zimepitisha mechi za kirafiki za FIFA au kuchagua viwanja mbadala vyenye sifa.

LIGI KUU YA VODACOM

Mechi namba 19: Coastal Union 2 v KMC 0- Klabu ya KMC imetozwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na timu yake kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 13, 2019 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. 
Mechi namba 24: Alliance FC 1 v Biashara United 1- Klabu ya Alliance imetozwa faini ya jumla ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na vurugu za washabiki wake pamoja na kufanya vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 20, 2019 Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Nayo klabu ya Biashara United imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kufanya vitendo vinavyoashiria imani ya ushirikiana wakati ikiingia uwanjani. Adhabu zote ni kwa mujibu wa Kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Mechi namba 40: Kagera Sugar 0 v Simba 2- Mchezaji Zawadi Mauya wa Kagera Sugar amepewa Onyo kutokana na kitendo chake cha kumpiga mateke mchezaji wa Simba kwenye mechi hiyo iliyochezwa Septemba 26, 2019 katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. 
 
Naye Mwamuzi wa mchezo huo Emmanuel Mwandembwa amepewa Onyo kwa kumuonesha Mauya kadi ya njano badala ya nyekundu kwa kitendo chake ambacho kilikuwa cha makusudi na kujirudia.

Mechi namba 41: Singida United 0 v Alliance FC 2- Klabu ya Alliance imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumweka kwenye benchi la ufundi Meneja ambaye hakutambulishwa katika kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) wakati wa mechi hiyo iliyofanyika Septemba 28, 2019 Uwanja wa Namfua mjini Singida. 

Mechi namba 44: Lipuli FC 2 v Tanzania Prisons 2- Klabu ya Tanzania Prisons imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kutokana na basi lililobeba wachezaji wa timu hiyo kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 29, 2019 Uwanja wa Samora mjini Iringa.