Jumanne , 10th Mei , 2016

Klabu ya Azam FC imekata rufaa, kupinga uamuzi wa kunyang'anywa pointi tatu katika mchezo wake dhidi ya Mbeya City na pointi hizo kupewa Mbeya City.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) Alfred Lucas amesema, wamepokea barua kutoka Azam FC ikipinga uamuzi huo mara baada ya Azam FC kukamilisha na kufuata taratibu zote za kanuni zinavyoagiza namna ya kukata rufaa.

Azam FC iliondolewa pointi tatu na kupewa timu ya Mbeya City Mei 05 mwaka huu bara baada ya kumtumia beki wao Erasto Nyoni aliyekuwa na kadi tatu za njano.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema katika mechi namba 156 iliyozikutanisha Mbeya City dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Azam ilimchezesha Nyoni kinyume na sheria huku wakitambua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Lucas alisema, Nyoni alipata kadi ya kwanza ya njano katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliowakutanisha Azam FC dhidi ya Yanga Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku kadi ya pili akiipata katika mchezo dhidi ya Coastal Union na kadi ya tatu akiipata katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa kwanza wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons.

Kwa mujibu wa uongozi wa Azam FC wenyewe ulisema katika taarifa iliyotolewa na TFF kuhusu kadi hizo haikuwa sahihi kwani Erasto alikuwa na kadi mbili za njano wakati akicheza mchezo dhidi ya Mbeya City na kadi ya njano ya tatu alikuja kuipata katika mchezo wa marudiano dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na sio katika mchezo wa kwanza kama ambavyo TFF imesema kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa Chamazi jijini Dar es Salaam waliopata kadi ni Beki Paschal Wawa na mshambuliaji Farid Mussa.