Azam FC yashindwa kuipiku Yanga

Jumatatu , 12th Feb , 2018

Klabu ya soka ya Azam FC imelazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara uliomalizika jioni hii kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kagera Sugar ndio walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 49 kupitia kwa Juma Shemvuni kabla ya Azam FC kusawazisha kupitia kwa Idd Kipagwile dakika 53.

Matokeo hayo ya mchezo wa raundi ya 18 yameiacha Azam FC katika nafasi ya tatu ikiwa imeongeza alama moja na kufikisha 34 sawa na Yanga iliyopo nafasi ya pili zikipishana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kwa upande wa Kagera Sugar imefikisha alama 14 na kuendelea kubaki katika nafasi ya 15, nafasi moja kutoka mwishoni mwa msimamo. Ligi kuu itaendelea tena siku ya Jumatano kwa michezo mbalimbali kupigwa.