
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi amesema wamefanikiwa kuzisoma timu zote za Bidvest Wits ya Afrika Kusini na Light Stars ya Shelisheli ambao Jumamosi iliyopita walicheza mchezo wa raundi ya awali ya michuano hiyo, ambao Bidvest Wits walishinda mabao 3-0.
Kitambi amesema dhumuni la kwenda huko ni kutaka kuwaona wapinzani watakaocheza nao katika raundi inayofuata na hata walipokwenda walikuwa wanajua kuwa watakutana na Bidvest katika raundi ijayo kutokana na aina ya mpinzani waliyekutana naye lakini walikuwa wakitaka kuhakikisha.
Kitambi amesema kwa sasa wanachoangalia zaidi ni kusafiri tena kuelekea Afrika Kusini kuwasoma tena Bidvest Wits katika moja ya mechi yao ligi, ili kuwasoma zaidi wapinzani wao hao wanaofundishwa na Gavin Hunt.
Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo, Azam FC ndiyo timu pekee ya Afrika Mashariki iliyoanzia raundi ya kwanza, ambapo itaanzia ugenini kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya moja ya timu hizo kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kumalizia nyumbani kati ya Machi 18, 19 na 20.