Azam FC yazichimba mkwara Simba na Yanga

Jumanne , 13th Feb , 2018

Baada ya kutofanya vizuri kwenye mechi mbili zilizopita, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Cheche, ameweka wazi kuwa huo si mwisho wa timu hiyo kwenye vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu kwani hata vinara Simba na Yanga wanaweza kufungwa.

Katika mechi nne zilizopita za ligi Azam FC imefanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo mmoja dhidi ya Ndanda (3-1), ikipoteza dhidi ya Yanga (2-1) na Simba (1-0) kabla ya jana kutoka sare ugenini na Kagera Sugar (1-1).

“Sisi tunasema bado tunamechi nyingi kwa sababu kupoteza mechi moja au mbili sio kukosa ubingwa ni kama vile mtu kuumwa ambapo kuumwa sio kufa, unaumwa unajiangalia nini tatizo unalifanyia kazi unajaribu kupambana upone na Yanga na Simba nao wanaweza kupoteza'', amesema kkocha msaidizi Idd Cheche.

Matokeo hayo kiujumla yameifanya Azam FC kufikisha pointi 34 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo sawa na Yanga iliyonafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 41, zote mbili zikiwa na mchezo mmoja mkononi.

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari kuelekea mkoani Iringa,kesho Jumatano alfajiri kwaajili ya kucheza na Lipuli kwenye mchezo wa raundi ya 19 Ijumaa jioni.