Jumamosi , 4th Jun , 2016

Baadha ya kusuasua kwa misimu kadhaa sasa tangu kuondoka kwa kocha Ferguson na makocha kadhaa kupita klabuni Manchester United sasa timu hiyo imeanza mikakati ya kurejesha enzi za kocha huyo aliyeipa mafanikio katika soka Barani Ulaya na duniani kote

Mshambuliaji Zlatan Ibrahimovic akishangilia moja ya mabao yake akiwa PSG.

Mashetani wekundu wa Old Trafold timu ya Manchester United wanataraji kukamilisha usajili wa mshambuliaji ngongoti mwenye uwezo mkubwa wa kupasua nyavu Zlatan Ibrahimovic na dili hilo litakamilika wakati wowote kuanzia sasa kabla ya michuano ya mataifa ya Ulaya [Euro 2016] haijaanza.

imefahamika kuwa kwa sasa Mtendaji Mkuu na Makamu wa Mwenyekiti wa klabu hiyo ya United Ed Woodward na wawakilishi wa Ibrahimovic wako katika kukamilisha masuala mbalimbali ya mkataba huo ambao unataraji kuwa wa mwaka mmoja.

Usajili huo utakuwa ni wa kwanza kwa kocha Mreno Jose Mourinho akimsajili mchezaji huyo wa kimataifa raia wa Sweden ndani ya viunga vya Old Trafford.

Na usajili huo wa mchezaji huyo huru baada ya kumaliza mkataba wake na matajiri wa Ufaransa Paris Saint-Germain dili lake litakamilika wakati wowote kabla ya Sweden haijashuka Dimbani kucheza mchezo wake wa kwanza wa kundi E Juni 13 mwaka huu kwa kupambana na timu ya Ireland.

Wakati huo huo Klabu ya Manchester United sasa wamepania kurejesha heshima yao baada ya kuwasilisha maombi mengine kwa mara ya pili ndani ya wiki tatu kwenye klabu ya Barcelona kutaka kumsajili mshambuliaji Muargentina Lionel Messi.

Klabu hiyo maarufu duniani, inataka kurejesha heshima na kucheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kama ilivyokuwa katika enzi za Mscotish Sir Alex Ferguson.

Imeelezwa Messi hana raha Hispania baada ya kuandamwa na kesi za masuala ya kodi. Kesi hizo bado zingali zikiendelea.

Manchester United imewasilisha mara mbili ndani ya wiki tatu maombi ya kumtaka Messi.

Kama itafanikiwa bado italipa kiasi kikubwa cha uhamisho kuliko kile Real Madrid walicholipa kumpata Gareth Bale kutoka Tottenham.

Man United tayari imemnasa Kocha maarufu Jose Mourinho ikionekana ni sehemu ya kutaka kurejesha heshima yake.