Jumanne , 10th Dec , 2019

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba Mohammed Dewji, ameahidi kutoa shilingi Milioni 100, kama zawadi kwa timu ya taifa ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars endapo itatwaa ubingwa wa CECAFA.

Mohammed Dewji

Mo Dewji ameyasema hayo jana usiku, alipotembelea kambi ya timu hiyo nchini Uganda, ambako michuano hiyo inafanyika, na kuwataka wachezaji wajitume zaidi ili waweze kupata ubingwa huo.

'Kama Mtanzania ambaye napenda kuona nchi yangu inafanya vizuri kwenye mchezo wa soka nimeahidi kutoa zawadi ya Tsh. 100m na zawadi ya pikipiki za Boxer kwa wachezaji na benchi la ufundi la timu yetu ya Tanzania Bara iwapo itashinda ubingwa wa michuano ya Cecafa ambayo inafanyika hapa nchini Uganda', alisema Mo Dewji.

Hatua hiyo ya kuahidi kiasi hicho cha pesa, imekuja siku moja baada ya kuahidi kutoa Milioni 500 kwenye awamu ya pili ya ujenzi wa uwanja wa Bunju Complex ambao umepewa jina la MO Simba Arena.

Ahadi hiyo alitoa siku ya Jumapili Desemba 8, 2019 kwenye mkutano mkuu wa Simba uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.

Kilimanjaro Stars leo inacheza na Zanzibar Heroes ukiwa ni mchezo wa pili baada ya ule wa kwanza kufungwa 1-0 na Kenya.