Jumatatu , 3rd Dec , 2018

Klabu ya soka ya Mtibwa Sugar ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, wana kibarua cha kusaka taji hilo mbele ya mabingwa wapya Raja Casablanca ambao wametwaa ubingwa huo jana usiku.

Kikosi cha Mtibwa Sugar, chini kulia ni wachezaji wa Raja Casablanca wakishangilia ubingwa.

Raja Casablanca wameibuka mabingwa wa kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2018 licha ya kufungwa mabao 3-1 na AS Vita Club ya DR Congo kwenye mchezo wa fainali ya pili uliopigwa usiku wa kuamkia leo.

Raja imebebwa na ushindi wa mabao 3-0 ilioupata kwenye fainali ya kwanza hivyo kuwa na ushindi wa jumla ya mabao 4-3 na kutawazwa kuwa mabingwa ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu walipofanya hivyo miaka 15 iliyopita.

Kwa upande wa kocha wa Casablanca, Juan Carlos Garrido yeye amekuwa kocha wa kwanza kuchukua kombe la shirikisho akiwa na vilabu viwili tofauti baada ya kufanya hivyo akiwa na Al Ahly ya Misri mwaka 2014.

Mtibwa ambao wapo kwenye michuano hiyo walishinda 4-0, mchezo wao wa kwanza raundi ya awali dhidi ya Northern Dynamo ya Ushelisheli na tayari wameshasafiri kwenda kwenye mchezo wa marejeano utakaopigwa Jumatano Disemba 5.

Kwa upande wa klabu bingwa tayari Simba wameshajua klabu inayoshikilia taji hilo ambayo ni Esperance ya Tunisia. Simba nao wapo nchini eSwatini kurudiana na Mbabane Swallows ambao waliwafunga mabao 4-1.