Bball Kings yatoa wawakilishi 'Giants of Africa'

Jumatano , 15th Aug , 2018

Michuano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings imeendelea kufungua milango kwa wachezaji wa mchezo huo baada ya vijana watatu kuwa miongoni wa vijana 13 kutoka Tanzania waliopata nafasi ya kwenda kwenye Kambi ya 'Giants of Africa' inayofanyika Nairobi, Kenya.

Moja ya michezo ya Sprite Bball KIngs

Taarifa ya shirikisho la mpira wa Kikapu nchini (TBF), imebainisha hilo baada ya kutaja majina 13 ya vijana wanaoshiriki kambi hiyo iliyoanza leo Agosti 15 hadi 20, 2018. Kambi hiyo inaandaliwa na Rais wa timu ya Toronto Raptors inayoshiriki ligi kuu ya Kikapu nchini Marekani NBA Masai Ujiri.

Katika vijana hao 13 yupo Atiki Ally Atiki ambaye amefanya vizuri kwenye Sprite Bball Kings na timu  ya Portland ambayo iliishia nusu fainali kwa kuondolewa na Mchenga Bball Stars. Pia mchezaji Quraish Slyvester Mganga ameichezea Water Institute iliyotolewa na Flying Dribblers kwenye robo fainali ya Sprite Bball Kings.

Mchezaji wa tatu katika orodha hiyo inayoongozwa na kocha Bahati Moses Mgunda ni Joseph Peter Sanka, ambaye alichezea mabingwa wa Sprite Bball Kings  mwaka jana Mchenga Bball Stars. Kambi hiyo ni maalum kwa kusaka vipaji na kuwapa nafasi ya kucheza NBA kwa wale ambao huibuka vinara.

Katika hatua nyingine TBF pia imeeleza kuwa timu ya Taifa ya chini ya miaka 18 itashiriki mashindano ya Afrika yatakayofanyika nchini Mali ya 3x3 kwa wanaume mwezi Septemba mwaka huu. 

Sprite Bball Kings yenyewe ipo katika hatua ya fainali ambapo game 5 za hatua hiyo zitaanza kupigwa Jumamosi Agosti 18, 2018 kati ya Flying Dribblers na mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars kwenye uwanja wa taifa wa ndani.

Orodha kamili.

1. Bahati Moses Mgunda (Kocha) 
2. Atiki Ally Atiki  
3. Omar Maalim Omari  
4. Quraish Slyvester Mganga 
5. Hossam Rashid Kitila 
6. Josephat Peter Sanka 
7. Noela Uwandameno 
8. Jesca Ngisaise Ong’Anyi 
9. Judith Pantaleo 
10. Anna Saileou 
11. Catherine Loishiye 
12. Mary Robert 
13. Husna Mohamed 
14. Neema Jonas