Jumatatu , 23rd Mei , 2016

Bodi ya ligi Tanzania TPLB imesema ligi kuu ya Tanzania bara iliyoamalizika hapo jana ilikuwa na ushindani mkubwa kwa timu japo kulikuwa na changamoto nyingi katika masuala tofauti katika ligi hiyo ambayo bingwa wake ni Yanga.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) Boniface Wambura.

Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo Boniface Wambura amesema wanataraji msimu ujao wa ligi hiyo watakuwa kwa kiasi kikubwa wamerekebisha mapungufu na changamoto zote zikiwemo suala la ratiba, nidhamu, waamuzi na ubovu wa viwanja.

Jambo linguine pia ni suala la upungufu wa mashabiki viwanjani nalo ni moja la suala ambalo Wambura amesema linahitaji mjadala mpana kujua ni nini sababu ya mashabiki kushindwa kujitokeza viwanjani msimu huu na nini sasa kifanyike msimu ujao ili kuondokana na tatizo hilo.

Aidha Wambura ambaye aliwahi kuwa Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF na pia Mkurugenzi wa Mashindano amesema pamoja na ligi kuu kuhitimishwa hapo juzi, lakini kuna mambo muhimu ya kukamilisha msimu huo akitaja kuwepo kwa hafla maalumu ya utoaji wa tuzo na zawadi mbalimbali kwa timu zilizofanya vema katika nafasi za juu na zawadi nyingine za ugungaji bora, mchezaji bora, kipa bora, beki bora, mchezaji bora chipukizi, mchezaji bora wa kulipwa [wakigeni] na nyingine nyingi kama timu yenye nidhamu, timu bora ya mwaka, kocha bora, mwamuzi bora.

Akimalizia Wambuara amesema bodi yake kwa kushirikiana na TFF wanataraji kukutana wakati wowote ndani ya wiki mbili zijazo kwa ajili ya kikao cha pamoja kujadili msimu huu wa ligi na ujao lakini pia kujipanga na halfa ya kufunga msimu wa ligi rasmi.