Bodi ya ligi yatoa adhabu, kocha wa Simba aguswa

Alhamisi , 13th Feb , 2020

Kamati ya Maadili ya Bodi ya Ligi imetoa mapitio ya makosa yaliyofanyika katika michezo ya hivi karibuni na kutoa adhabu mbalimbali kwa wahusika ambao walikiuka kanuni na taratibu za uendeshaji wa soka nchini.

Kocha Sven Vanderbroeck

Kikao hicho cha Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichokaa Februari 10,2020 kimetoa maamuzi ya kumpa onyo kali kocha wa Simba, Sven Vanderbroeck kwa kosa la kugoma kuwafungulia mlango mwamuzi na Kamishina wa mchezo wakati wa ukaguzi wa timu katika mechi dhidi ya Coastal Union, Februari  01, 2020 katika uwanja wa Taifa. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni namba 41(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.

Polisi Tanzania imepigwa Faini ya Tsh.1,500,000/= (Milioni Moja na Laki Tano) kwa kosa la kutumia mlango usio rasmi wa kuingia uwanjani katika mechi iliyochezwa Februari 04, 2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Adhabu iliyotolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(14) ya Ligi Kuu.

Aidha katika maamuzi hayo, mwamuzi Abubakar Mturo amefungiwa miezi mitatu (3) kwa kosa la kushindwa kumudu mchezo katika mechi iliyochezwa Februari 05,2020 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni namba 39(1) ya Ligi Kuu Kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.