Alhamisi , 9th Jul , 2020

Mwana masumbwi maarufu nchini Tanzania,Hassan Mwakinyo amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli kuunga mkono jitihada za mabondia kama ambavyo amefanya mambo makubwa kwenye sekta nyingine,ili kuwapa morari wao kufanya vyema na kuitangaza nchi .

Bondia Hassan Mwakinyo (Pichani kati kati) akiwa ulingoni katika moja ya pigano lake.

Mwakinyo ametoa kauli hiyo akiwa katika matayarisho ya pambano la kimataifa dhidi ya bondia Tshibangu Kayembe raia wa Congo lililopangwa kufanyika Agosti 14 mwaka huu katika  ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam.

Akizungumzia pambano hilo Mwakinyo amesema amejiandaa vyema kuelekea pambano hilo la kuwania ubingwa wa WBF ili aweze kuipeperusha bendra ya Taifa na hatokubali kuiangusha nchi.

Ikumbuke Mwakinyo amepanda ulingoni katika mapambano 18 na kapoteza mara mbili tu huku mpinzani wake amecheza mapambano 12 na kushinda 9 huku akitoka sare mara 3.

Kwa upande wa mratibu wa pambano hilo  Beautrice Said amesema kutakua na mapambano ya utangulizi yakiwemo  la Seleman Kidunda atakayeumana na Shaaban Kaoneka uzito wa Kg 72, Issa Nampepecha na Khaleed Manjee Kg 61.

Pigano jingine la kimataifa ambalo ni la raundi 12 litawakutanisha mkenya Gabriel Ochieng na Tony Rahid ikiwa ni la ubingwa wa ABU.