Alhamisi , 1st Jan , 2015

Chama cha Mpira wa Netball nchini CHANETA, kimesema mwaka huu kinaanza kuwa na mpango mkakati wa kukuza vipaji vya vijana ili kupata timu nzuri za shuleni.

Akizungumza na East Africa Radio, Mwenyekiti wa CHANETA, Anna Kibira amesema mpango huo utaanzia katika ngazi za vijiji na kumalizia mashuleni.

Kibira amesema, wana imani zoezi hilo litafanikiwa kutokana na kukamilika miundombinu ya mchezo huo kwa mikoani ambapo mpaka sasa wana viwanja 600 vya mpira wa Netball mjini Mtwara, Lindi na Shinyanga.

Kibira amesema, mpango wa kuanza kutafuta vijana hao utajadiliwa katika mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi mwaka huu ili kuweza kujua mikoa yenye viwanja hivyo wanatumia vipi viwanja hivyo kukuza vipaji kwa vijana.

Kibira amesema, katika zoezi hilo wameshapata walimu na pia wameshatoa semina kwa walimu hao ambao wanaamini watakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo kwa vijana katika mchezo huo na kuweza kuwa timu nzuri.