Fahamu sababu za KMC kuitoa AS Kigali CAFCC

Jumatatu , 19th Aug , 2019

Kuelekea mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho barani Afrika kati ya KMC dhidi ya AS Kigali, klabu ya KMC inazo sababu za kuitoa timu hiyo ya Rwanda.

KMC

Usajili bora waliofanya ni moja ya sababu zinazoipa nafasi timu hiyo kufanya vizuri, wakiwa nyumbani baada ya kupata sare mjini Kigali.

KMC imewasajili wachezaji wazoefu na wenye uwezo kama mfungaji bora wa Mwadui msimu uliopita, Salim Aiyee, Ramadhani Kapera  Ndanda, Vitalis Mayanga, Jean Mugiraneza na Kenny Ally.

Uwepo wa kocha mzoefu raia wa Uganda, Jackson Mayanja. Kocha huyo amewahi kutengeneza timu kama Kagera Sugar zikawa tishio lakini pia amewahi kuifundisha Simba hivyo ana nafasi kubwa ya kuendelea kuifanya KMC kuwa timu bora.

Sababu nyingine inayoweza kuwapa matokeo mazuri KMC ni sare yao ugenini, ambapo nyumbani wanahitaji ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele.

Uongozi madhubuti wa KMC chini ya Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamin Sitta, umeonesha kuwa na mipango endelevu ikikumbukwa kuwa wakiwa katika msimu wao wa kwanza tu kwenye ligi kuu, wamefanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne na pia kufanya usajili mzuri kwaajili ya msimu ujao.

KMC itakuwa mwenyeji wa AS Kigali wikiendi hii, ambapo itatakiwa kushinda ili kusonga mbele katika michuano ya Kombe la shirikisho.