Jumanne , 13th Apr , 2021

Wababe wa nchini Ureno, Klabu ya FC Porto itajitupa dimbani saa 4:00 usiku wa leo tarehe 13 Aprili 2021 kukipiga dhidi ya matajiri wa jiji la London, klabu ya Chelsea kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.

Mshambuliaji wa FC Porto, Moussa Marega (kushoto) na mshambuliaji wa Chelsea, Timo Werner (kulia).

FC Porto wanakibarua kigumu cha kupindua matokeo baada ya kufungwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza huku kiungo wake tegemezi Sergio Oliveira akiwa mashakani kucheza mchezo huo kutokana na kutokuwa fiti lakini pia kutokana na ubora wa mpinzani wake Chelsea wa kutokupoteza mchezo hata mmoja kwenye michezo 9 ya michuano hiyo, akishinda michezo 7 na kutoa sare 2 pekee.

Akielezea hali ya nyota huyo, kocha wa FC Porto, Sergio Conceicao amesema “Kama unavyojua, mchezo wa mwisho hakuwa tayari kwa kucheza dakika 90 kwa sababu ya tatizo dogo la maumivu ya misuli kitu ambacho siku zote ni hali ya hatari”. Amesema kocha wa FC Porto,Conceicao.

(Kiungo mshambuliaji wa FC Porto, Sergio Oliveira )

Oliveira ni mchezaji muhimu zaidi kwenye kikosi hicho kwani amefunga mabao 17 na kutengeneza mabao 7 kwenye jumla ya michezo 40 aliyocheza kwenye michuano yote msimu huu.

Kwa upande wa Chelsea, kocha wa klabu hiyo, Thomas Tuchel ametoa hali ya kikosi kwa kumgusia kiungo wake mkabaji Ng'olo Kante kwa kusema bado yupo njia panda juu ya kumtumia mchezaji huyo kwenye mchezo wa usiku wa leo.

“Tunahitaji kuwa makini kuhusu yeye. Swali ni aidha tunamhitaji ananze mchezo au amalizie. Na hilo halina majibu yake kwa sasa, nitalifanyia maamuzi”. Tuchel.

Nae mlinzi wa kati mkongwe, Thiago Silva anatazamiwa kurejea kikosini baada ya kupona majeraha yake ya maumivu ya nyama za paja na huenda akaiongoza tena safu ya ulinzi ya Chelsea.

Wakati FC Porto akijiandaa kupindua meza ili kutinga hatua ya nusu fainali, rekodi zinaonesha kuwa, ni mara nne pekee timu zimesonga mbele hatua inayofuata kwenye mtoano ya michuano y a ligi ya mabingwa ulaya zikiwa zimepoteza mchezo wa mkondo wa kwanza bila kupata bao.

Huku Chelsea akiweka rekodi ya kupata ushindi kwenye mara 11 kwenye michezo yake ya mkondo wa kwanza kwenye michuano hiyo na kufanikiwa kusonga mbele mara nane kwenye awamu kumi na kufeli dhidi ya Barcelona mwaka 199-2000 na Liverpool mwaka 2006-2007.

Mshindi wa jumla wa Chelsea na FC Porto atacheza na mshindi wa jumla kati ya Real Madrid na Liverpool kwenye hatua ya nusu fainali mwezi Mei.