Flying Dribblers wapewa siri ya ushindi

Jumanne , 21st Aug , 2018

Timu ya Flying Dribblers ambayo inacheza fainali ya michuano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings 2018 dhidi ya mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars, imepewa mbinu za kutumia kwenye game 2 baada ya kupoteza game 1.

Mchezaji Baraka Mopele wa Flying Dribblers mwenye jezi namba 2 akiwa anataka kufunga kwenye game 1 dhidi ya Mchenga.

Mchezaji na mchambuzi wa mchezo wa Kikapu Ladislaus Ikungura, ameeleza kuwa mapungufu pekee ya Flying Dribblers yalikuwa ni kushindwa kuwa na mbinu za kumdhibiti nyota wa Mchenga Baraka Sadick kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuzuia mipira isimfikie.

''Flying walishindwa kumchezea 'double team' Baraka pia kukataza mpira usimfikie kwa kulazimisha mpira uende kwa mtu mwingine tofauti na yeye kwani tayari walikuwa wameshajua ndio mtu hatari kwao'', amesema.

Pia kwa upande mwingine ameeleza kuwa kushindwa kutumia nafasi vizuri nako kuliwagharimu Flying katika game 1 ambapo katika mitupo huru 'free throw' 29 waliyopata walifunga 16 pekee huku wapinzani wao kwa kupitia Baraka huyo huyo wakatumia vizuri nafasi kama hizo.

Kuelekea game 2 itakayopigwa kesho kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay Flying Dribblers wanatakiwa kuongeza idadi ya watu wanaoweza kufunga ili kwenda sawa na Mchenga ambao walikuwa na watu wengi wa kufunga ukiacha Baraka aliyefunga pointi 48, kulikuwa na wachezaji wengine waliofunga zaidi ya pointi 15.

Katika game 1 ya 'best of five' za fainali iliyopigwa Agosti 18 kwenye uwanja wa taifa wa ndani na kumalizika kwa Mchenga kushinda kwa pointi 103 kwa 73. Mchenga walitumia vizuri 'free throw' zao kwa kufunga 23 kati ya 24.