Hali ni mbaya, nini hatma Aston Villa ya Samatta

Jumanne , 10th Mar , 2020

Matumaini ya Aston Villa kusalia katika Ligi Kuu nchini Uingereza yanazidi kudidimia siku hadi siku, baada ya hapo jana kupokea kichapo kingine kizito kutoka kwa Leicester City.

Mbwana Samatta na mlinzi wa Leicester City, John Evans

Katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa nyumbani wa Leicester, King Power, ilishuhudiwa Aston Villa ikinyukwa mabao 4-0 na kuifanya kuendelea kusalia katika nafasi mbaya ya 19 ya msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 28.

Villa inakabiliwa na michezo migumu kuelekea mwishoni mwa ligi, ikiwa imebakiza mechi 10, ambapo mechi sita kati ya hizo watakutana na vigogo wa ligi hiyo Chelsea, Wolves, Liverpool, Manchester United, Arsenal na Everton.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Mtanzania Mbwana Samatta aliyejiunga katika dirisha dogo la usajili la Januari, ana kazi kubwa ya kufanya na wenzake ili kujikwamua kutoka katika janga hilo. Vinginevyo yeye mwenyewe aoneshe kiwango kizuri pamoja na kufunga mabao ya kutosha ili azivutie timu zingine zitakazobaki kwenye ligi endapo Aston Villa itaporomoka daraja.