Jumanne , 24th Jul , 2018

Moja ya malengo ya michuano ya Sprite Bball Kings inayoandaliwa na East Africa Television LTD kwa udhamini wa kinywaji cha Sprite ni kuinua vipaji, tayari wakali mbalimbali katika maeneo tofauti wameshaanza kuonekana kuanzia hatua ya mchujo mpaka robo fainali.

Timu za Mchenga Bball Stars na St. Joseph kwenye mechi yao ya robo fainali.

Tayari michuano hiyo imeshafika hatua ya nusu fainali ambapo mechi 2 za hatua hiyo zitapigwa Jumapili hii ya Julai 29, kwenye uwanja wa ndani wa taifa. Hawa ndio wachezaji watatu wanaoongoza kwa kufunga pointi nyingi kwenye mechi tatu walizocheza hadi sasa ambazo ni hatua ya mchujo, hatua ya 16 bora na robo fainali. 

Namba moja imeshikiliwa na mchezaji David Godfrey wa St. Joseph, ambaye amefunga pointi 92, akianza a pointi 19 kwenye haua ya mchujo, pointi 41 kwenye 16 bora na kumaliza kwa pointi 32 kwenye robo fainali. Bahati mbaya timu yake imetolewa kwenye mashindano katika hatua ya robo fainali.

Kutoka kushoto ni Baraka Mopele wa Flying Dribblers, Denis Babu wa Portland (katikati) na David Godfrey wa St, Joseph (kulia).

Namba mbili inashikiliwa na nahodha wa Portland, Denis Babu ambaye amefunga jumla ya pointi 74. Babu alianza kwa kufunga pointi 19 kwenye mechi za mchujo kabla ya kufunga pointi 24 kwenye hatua ya 16 bora na robo fainali amefunga pointi 31. Timu yake ya Portland imetinga hatua ya nusu fainali.

Namba tatu amesimama Baraka Mopele wa Flying Dribblers ambaye amefunga pointi 71. Alianza na pointi 8 kwenye hatua ya mchujo, kisha akafunga pointi 38 kwenye 16 bora na robo fainali amefunga pointi 25. Timu yake imefuzu nusu fainali ya michuano hiyo.