Klabu Bingwa Ulaya
Mechi nane zitapigwa leo ambapo mechi za mapema kabisa, Lyon itawakaribisha Zenit St. Petersburg, Inter dhidi ya Slavia Prague, na Ajax dhidi ya Lille. Mechi za baadaye, Napoli itakuwa nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool, Benfica dhidi ya RB Leipzig, Chelsea dhidi ya Valencia, Dortmund dhidi Barcelona na Salzburg ikicheza na Genk.
Mshambuliaji wa klabu ya Genk na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ataweka historia kubwa usiku wa leo endapo atacheza, ambapo atakuwa mchezaji wa kwanza Tanzania kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, klabu yake itakapovaana na Salzburg.
Lakini kitu cha kuvutia zaidi katika michuano hii ni kwamba pamoja na umaarufu iliyonayo hivi sasa, zipo klabu ambazo kwa sasa zinashiriki madaraja ya chini katika nchi na ziliwahi kushinda ubingwa katika miaka ya nyuma, klabu hizo ni Nottingham Forest ya Uingereza na Hamburger SV ya Ujerumani.
Nottingham Forest ambayo kwa sasa inashiriki ligi daraja la kwanza nchini Uingereza, iliwahi kushinda ubingwa huo mwaka 1980 wakati huo ukiitwa 'European Cup' ambapo ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Hamburger SV na miaka mitatu baadaye mwaka 1983, Hamburger SV ambayo kwa sasa inashiriki ligi daraja la kwanza nchini Ujerumani ilishinda ubingwa kwa kuifunga Juventus katika fainali kwa bao 1-0.
Katika msimu huu, kila timu imeonesha namna ilivyojiandaa kushinda ubingwa kiasi kwamba ni vigumu kutabiri nani atashinda mbio hizo, ni suala la kusubiri.
