Jumatano , 11th Jul , 2018

Klabu ya manispaa ya Kinondoni (KMC), imejibu tuhuma dhidi yao ya kumsajili mchezaji Ally Ally kutoka Stand United wakati akiwa na mkataba wa miaka miwili na klabu yake.

KMC kupitia kwa mkurugenzi wake, Walter Urio imesema kuwa wamemsajili Ally Ally baada ya kujiridhisha kuwa yuko huru, alipovunja mkataba na klabu yake na ushahidi wanao huku wakiitaka Stand United ilete ushahidi wao mezani watawajibu.

“Sisi tumemsajili Ally Ally baada ya kujiridhisha kuwa yuko huru, alivunja mkataba na Stand United baada ya kudai malimbikizo ya mshahara wake wa miezi minne na ushahidi wa nakala ya barua ya kuvunja mkataba ipo SPUTANZA na TFF kwahiyo wao kama bado wanadai ni mchezaji wao basi wapeleke ushahidi TFF “. Amesema Urio.

Stand United kupitia kwa mwenyekiti wa kamati ya usajili, Mbasha Matutu ulionesha kusikitishwa juu ya usajili huo kwani hawakuwa na taarifa yoyote juu ya kuondoka kwake Shinyanga kuja Dar es salaam na kusaini KMC.

Matutu pia amekana tuhuma za kushindwa kumlipa mshahara wa miezi minne mchezaji huyo kuwa ni sababu iliyopelekea kuvunja mkataba naye huku akisisitiza kuwa wao walikuwa wakimlipa mshahara wake kila mwezi kama kawaida na hawana deni lolote kwake.

Ally Ally amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia klabu ya KMC ambayo imepanda kucheza ligi kuu Tanzania Bara kuanzia msimu ujao wa 2018/19.