Ijumaa , 17th Feb , 2023

Kocha wa Simba SC, Mbrazil Roberto Olivier ‘Robertinho’ amesema wamejipanga vizuri kuwakabili wapinzani wao klabu ya Raja Casablanca ya Morocco kwenye mchezo wao wa klabu bingwa Afrika unaotaraji kucheza Jumamosi ya kesho Februari 18, 2023 kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

Akizungumza na Wanahabari kuhusu maandalizi ya mchezo huo, Koha Robertinho amesema wamejipanga kupata ushindi na kupata alama 3 pekee huku akisisitiza kuwa wapinzani wao Raja ni timu bora wataingia kwa tahadhari zote.

"Nimewaandaa vizuri wachezaji wangu kuhakikisha tunapata pointi tatu katika mchezo huo na kuweza kuingia hatua ya makundi,amesema  Oliviera.

Kwa upande wa Nahodha wa Simba SC, John Rafael Bocco amesema anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa motisha kubwa aliyoitoa ya kuahidi kununua kila goli moja kwa shilingi milioni 5 na kuwafanya wapambane zaidi.

"Tunahitaji pointi tatu kwenye uwanja wa nyumbani Kocha wetu ametupa mbinu mbadala ambazo tunaamini zitatusaidia kwa kiasi kikubwa hapo kesho''amesema Bocco.

Simba SC ipo nafasi ya 3 kwenye kundi C ya michuano hiyo mikubwa Afrika baada ya kufungwa bao 1-0 kwenye mchezo wake wa kwanza na Mabingwa wa Guinea Klabu ya Horoya huku kinara akiwa Raja Casablanca ya Morocco na Vipers ya Uganda ikishika mkia.