Kocha timu ya taifa ampa dili mpya Kelvin John

Jumanne , 8th Oct , 2019

Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya vijana U20, Zuberi Katwila amempa nafasi mshambuliaji wa timu hiyo, Kelvin John kufanya mazoezi katika klabu yake ya Mtibwa Sugar.

Mshambuliaji wa timu ya taifa U 20, Kelvin John

Katwila ambaye amemfundisha Kelvin John katika michuano ya CECAFA U20 Challenge Cup iliyomalizika wikiendi iliyopita nchini Uganda, amesema kuwa anamfahamu vizuri mchezaji huyo na anajua malengo yake hivyo anampa nafasi ya kufanya mazoezi wakati akisubiri matokeo ya majaribio yake aliyofanya barani Ulaya.

"Ninamfahamu vizuri Kevin, ni kijana mwenye nidhamu na malengo. Ni tofauti kabisa na wachezaji wengine, nimezungumza naye nikamuuliza malengo yake katika soka akaniambia anataka kucheza Ulaya, hilo ni jambo jema kwa kijana wa umri wake kuwaza kwenda mbali zaidi", amesema Katwila.

"Kwa vile hana timu hapa nchini na sasa hivi anasubiri ripoti ya majaribio yake Ulaya, mimi namkaribisha Mtibwa Sugar aje afanye mazoezi na apate uzoefu", ameongeza.

Kelvin John ameibuka na tuzo mbili katika michuano hiyo ya Challenge iliyomalizika hivi karibuni, tuzo ya mchezaji bora wa mashindano na mfungaji bora akiwa na jumla ya mabao 7.